Breaking News

Simba yaonesha ubabe wao kwa yanga katika kuinasa saini ya Mwamnyeto.

VITA kubwa ya usajili imehamia kwa beki wa kati wa timu ya taifa, Taifa Stars na klabu ya Coastal Union, Bakari Mwamnyeto anayewaniwa vikali na klabu kongwe za Simba na Yanga katika usajili wa dirisha dogo, lakini mambo yanavyokwenda inaonekana Simba wanaelekea kuwazidi ujanja Yanga kwa kuwa ndio waliozungumza nao kwa mara ya mwisho.

Kumbuka kuwa dirisha dogo linanukia, limepangwa kufunguliwa katikati ya mwezi ujao. Awali, Yanga ndiyo ilikuwa ya kwanza kuwania saini ya beki huyo kwenye usajili mkubwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu kabla ya dirisha dogo kumfuata huku Simba ikitajwa kuingia kwenye vita ya kuitaka saini ya beki huyo.

Hiyo ni baada ya beki huyo kuonyesha kiwango kikubwa katika mchezo wa kwanza wa kuwania kufuzu Afcon walipocheza na Equatorial Guinea wakifanikiwa kuwafunga mabao 2-1 mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam huku Mwamnyeto akicheza kati pamoja na Kelvin Yondani.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, Simba inawania saini ya beki huyo kwa ajili ya kuiboresha safu yao ya ulinzi ambayo inamtegemea Erasto Nyoni na Muivory Coast, Pascal Wawa pekee.

Mtoa taarifa huyo alisema wanataka kumsajili beki huyo baada ya Mbrazili, Tairone Do Santos kuonekana Kocha Mkuu wa timu hiyo kutoridhishwa na kiwango chake ambacho amekionyesha kwenye baadhi ya mechi ambazo amemuanzisha katika kikosi cha kwanza kwenye ligi.

No comments