Breaking News

Kagere aweka rekodi mpya VPL

MSIMU uliopita mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere aliweka rekodi ya kufunga mechi mbili za kwanza kwenye Ligi Kuu Bara.
Mechi hizo ni dhidi ya Prisons waliposhinda bao 1-0 na Mbeya City ambapo Simba ilishinda mabao 2-0, yote yalifungwa na Kagere aliyemaliza msimu akiwa na magori 23 na kuibuka Mfungaji Bora msimu uliopita.
Mechi ya tatu msimu uliopita Simba walicheza na Lipuli ambayo ilimalizika kwa suluhu kwa maana hiyo Kagere alishindwa kufunga bao.
Msimu huu Kagere ameweka rekodi nyingine mpya kwa kufunga mechi zote tatu za kwanza ambazo Simba wamecheza mpaka sasa.
Mechi ya kwanza Simba walicheza na JKT Tanzania ambayo walishinda mabao 3-1, Kagere akiweka kambani mabao mawili.
Mechi ya pili Simba walicheza na Mtibwa Sugar, Kagere alifunga bao moja katika ushindi wa bao 2-1.
Mechi ya tatu Simba iliyochezwa jana Alhamisi wakiwa ugenini uwanja wa Kaitaba mjini  Bukoba dhidi ya Kagera Sugar ambao walikubali kipigo cha mabao 3-0.
Katika ushindi huo Kagere alifunga mabao mawili na kuweka rekodi ya kufunga mechi tatu za mwanzo msimu huu.
Mabao hayo mawili ambayo Kagere alifunga dhidi ya Kagera Sugar, yanakuwa mabao matano msimu huu lakini anatimiza jumla ya mabao 28, kwenye ligi ndani ya misimu miwili.

No comments